USAJILI: Dirisha Dogo la Usajili lafunguliwa Rasmi

Jana Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kupitia Mtendaji wake Mkuu Boniface Wambura, ilithibitisha kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili leo Alhamisi Novemba 15 2018.

Wambura alisema kulingana na kalenda ya mashindano, dirisha la usajili limefunguliwa leo na litafungwa Disemba 15.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo ligi ilikuwa ikisimama kipindi chote cha usajili wa dirisha dogo, mwaka huu ligi itaendelea.

“Ni kweli kwa kalenda ya mashindano November 15 hadi December 15 linafunguliwa dirisha dogo la usajili lakini ukiangalia ratiba yetu ligi haitasimama kupisha dirisha dogo la usajili,” alisema Wambura

“Ligi kuu imesimama kupisha kalenda ya FIFA kuanzia November 12 hadi 20, baada ya hapo kutakuwa na hatua za awali za Caf Champions League na Confederation Cup, ligi itaendelea kama kawaida.

“Nadhani December 2 ligi kuu inaendelea na daraja la kwanza na daraja la pili, kwa hiyo hatutasimama tutacheza kama ilivyokuwa msimu uliopita tunacheza huku watu wanaendelea na usajili wa dirisha dogo.”

“Tunazikumbusha timu, nadhani zinajua umuhimu wa dirisha dogo, kama kuna mahali kuna upungufu warekebishe kwa sababu ndio mahali ambapo kama timu yako imecheza mechi 15 za ligi benchi la ufundi litakuwa limepata mwelekeo kwamba liimarishe kikosi wapi”

Tayari baadhi ya timu zimetambulisha wachezajiwaliowasajili. Azam Fc imemtambulisha Obrey Chirwa huku KMC ikimtambulisha Elius Maguri

Kwa upande wa Yanga Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Hussein Nyika amesema timu hiyo inaendelea na mchakato wa kukamilisha usajili wa wachezaji waliopendekezwa na kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera.