Yanga haikufanya usajili wa maana katika dirisha dogo la lililofungwa wiki iliyopita na kuacha malalamiko mengi kwa viongozi wa timu hiyo.
Kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ ndio mchezaji pekee ambaye alipendekezwa na Kocha Mwinyi Zahera aliyefanikiwa kusajiliwa.
Zahera aliutupia lawama uongozi wa Yanga kwa kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji wengine wanne huku akikerwa na kitendo cha uongozi wa timu hiyo kumdanganya kuwa usajili wa wachezaji hao ungekamilika
Lakini Mcongomani huyo amesema atatumia wachezaji waliopo ingawa hawezi kutoa ahadi ya kutwaa ubingwa.
Hata hivyo kushindwa kwa usajili wa wachezaji wapya kunaweza kuwa chachu ya kuwafanya wachezaji waliopo waongeze bidii zaidi ili kumshawishi kocha juu ya uwezo wao.
Ujio wa wachezaji wapya pengine ungeweza kuwaondoa baadhi ya wachezaji kikosini lakini sasa watakuwa na nafasi nyingine ya kumshawishi Zahera
Wachezaji hawa waliopo katika kikosi cha Yanga hawapaswi kukatishwa tamaa kwa kuhofia kuwa timu haitafanya vizuri eti kwa kuwa usajili uliopendekezwa haukufanikiwa
Hakuna ubishi kama wachezaji waliotakiwa na Zahera wangesajiliwa, Yanga ingekuwa moto zaidi lakini hata sasa ikiwa na hawa wachezaji waliopo Yanga haikamatiki
Wachezaji waliopo wameiwezesha Yanga kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi wakiongoza kwa tofauti ya alama nne dhidi ya Azam FC na alama 17 dhidi ya Simba inayojinasibu kuwa na kikosi cha zaidi ya Bil 1
Kama ilivyowashangaza wale ambao mwanzoni mwa msimu walikuwa wakiamini na wengine kudiriki kusema ‘Msimu huu Yanga inapigania isishuke daraja’, basi mwishoni mwa msimu pia Yanga itawashangaza wale wanaoamini kushindikana kwa usajili wa wachezaji wapya kutaigharimu timu hiyo.
Kitu pekee kinachoweza kuigharimu Yanga sasa ni labda akiondoka kocha Mwinyi Zahera ambaye amekuwa akifanya kazi ya ziada kuhakikisha timu inafanya vizuri.