
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji baada ya kutembelewa na Waziri Mkuu katika kambi ya kikosi cha Stars, Samatta amesema wanajiona kuwa na deni kubwa kwa Watanzania na watahakikisha wanawapa furaha kwa kupata ushindi leo
“Naona naenda kuiongoza nchi siku ya kesho (leo), sitakuwa nahodha kwa ajili ya wachezaji peke yake bali nitakuwa nahodha kwa ajili ya wananchi wote wa Tanzania,” amesema Samatta
“Wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya kuitetea nchi yao, lengo kubwa ni kuhakikisha bendera yetu ya Tanzania inasimama, Dunia itambue na Afrika yote ifahamu”
Jana Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa alitembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa na kuwaeleza kwamba Serikali na wananchi wanamatumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda leo
“Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho (leo) na Serikali inamatumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo muelewe kwamba kesho (leo) ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia”