Mabadiliko makubwa ya kikosi yanakuja Yanga

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amepania hasa kutengeneza kikosi imara ili msimu ujao kuwa na timu itakayotoa ushindani wa kweli kwenye ligi na kwa wapinzani wake Simba ambao kwa msimu wa pili sasa wanaonekana kukosa changamoto

Baada ya kuhakikishiwa ‘fungu la uhakika’ kwa ajili ya kufanya usajili, Zahera amepanga kutengeneza Yanga mpya mapema tu ili wakati anaondoka kwenda Congo kwa ajili ya michuano ya AFCON 2019, aache masuala ya usajili yawe yamemalizika

Mcongomani huyo ana mwezi mmoja tu wa kukamilisha michakato hiyo ambayo tayari imeshaanza kukamilishwa kwa usiri mkubwa

Zahera amepania kufanya mabadiliko makubwa kwenye baadhi ya maeneo ambayo mwenyewe aliyaanisha kuwa na mapungufu

Golikipa

Baada ya ‘kumtosa’ Beno Kakolanya aliyeingia kwenye mgogoro na uongozi, Yanga itasajili mlinda lango mwingine kuziba nafasi yake ambaye atasaidiana na Klaus Kindoki na Ramadhani Kabwili.

Hata hivyo Kabwili nae anawaniwa na timu kutoka Saudi Arabia

Mlindalango wa Bandari Fc Farouq Shikalo anatajwa kuwa kwenye mazungumzo na Yanga

Walinzi wa pembeni

Yanga huenda ikasajili walinzi wawili wa pembeni, mmoja wa kulia mwingine wa kushoto ili kuwaongezea nguvu waliopo

Kwa sasa Yanga inawategemea zaidi Gadiel Michael na Paulo Godfrey huku hatma ya Juma Abdul na Haji Mwinyi ikibaki mikononi mwa Zahera

Mikataba ya wakongwe hao katika kikosi cha Yanga inamalizika mwishoni mwa msimu

Mlinzi wa kati

Eneo la safu ya ulinzi wa kati linatarajiwa kuboreshwa kwa kuongeza mlinzi mwingine licha ya eneo hilo kuwa na walinzi watatu wa kutegemewa Kelvin Yondani, Andrew Vicent na Abdallah Shaibu ‘Ninja’

Mlinzi wa AS Vita Yanick Bangala ambaye yuko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo anatajwa kuwaniwa ili kuongeza nguvu kwenye safu hiyo

Kiungo Mkabaji

Papi Tshishimbi alisajiliwa na Yanga kucheza nafasi ya kiungo mkabaji.

Hata hivyo alipokuja Zahera alimbadilishia majukumu kwa kumchezesha namba 10 au 8 nafasi ambazo amekuwa akifanya vizuri

Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekuwa akitumika nafasi ya kiungo mkabaji lakini Zahera alisema analazimika kumtumia kinda huyo kwa kuwa ndiye anayemudu zaidi nafasi hiyo kuliko viungo wengine

Lakini Fei Toto alipaswa kucheza namba nane, na ndio nafasi ambayo kocha wa timu ya Taifa Emmanuel Amunike amekuwa akimtumia kwenye kikosi cha Stars

Yanga huenda ikasajili kiungo mkabaji ‘wa asili’ ambaye pia atakuwa na uwezo wa kucheza nafasi ya ulinzi wa kati

Washambuliaji wa pembeni

Zahera ni muumini wa soka la kushambulia kwa kasi kupitia pembeni na mara kwa mara amelalamika kuwa Yanga haina wachezaji wa nafasi hiyo wanaoendana na mfumo wake na hivyo ndio sababu inayomfanya afanye mabadiliko ya mara kwa mara pembeni

Ni Mrisho Ngasa pekee ambaye kwa sasa amejihakikishia namba kwenye kikosi cha Zahera miongoni mwa washambuliaji wanaotokea pembeni

Yanga huenda ikaongeza viungo washambuliaji wawili wa pembeni kwa kila upande

Safu ya ushambuliaji

Yanga ina washambuliaji wa asili wawili tu, Amissi Tambwe na Heritier Makambo.

Wakati hatma ya Tambwe ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu ikibaki mikononi mwa Zahera, hakuna shaka, safu ya ushambuliaji itaongezewa nguvu

Miongoni mwa washambuliaji wanaotajwa kuwaniwa na Yanga ni Jackues Tuyisenge ambaye mkataba wake na Gor Mahia uko ukiongoni huku ‘mtukutu’ Obrey Chirwa akitajwa kuwa tayari kurejea Yanga baada ya kugoma kuongeza mkataba na Azam Fc. Makataba wake wa miezi sita unamalizika mwishoni mwa msimu

Juzi Zahera alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema kikosi chake cha msimu ujao kitakuwa na mabadiliko makubwa sana, wachezaji wa zamani ambao wataendelea kubaki Yanga hawatazidi 10