Yanga kuanza mawindo ya Azam Fc Jumanne

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea mazoezini kesho Jumanne kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam Fc utakaopigwa Jumatano ijayo April 29 katika uwanja wa Taifa

Kocha Mkuu wa vinara hao wa ligi Mwinyi Zahera aliwapa wachezaji siku tatu za mapumziko ili washeherekee sikukuu ya Pasaka wakiwa na familia zao

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema baada ya mapumziko hayo, kesho wataanza kujifua uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kujiandaa na mchezo huo

Yanga bado haijakata tamaa katika mbio za kuwania ubingwa licha ya watani zao Simba kuwa na idadi kubwa ya michezo ya viporo ambayo kama watashinda yote, watatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Juzi Zahera alisema hesabu zao ni kushinda michezo yote sita iliyobaki huku akiamini wapinzani wao Simba wataendelea kudondosha pointi hivyo kuwapa mwanya wa kutwaa ubingwa

Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imejukusanyia alama 74 baada ya kushuka dimbani mara 32.

Inafuatiwa na Azam Fc yenye alama 66 ikiwa imeshuka dimbani mara 32 pia. Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 60 ilizovuna katika michezo 24