Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga Charles Mkwasa anaamini timu hiyo inahitaji maboresha katika baadhi ya nafasi ili iweze kuchuana na Simba msimu ujao katika kuwania ubingwa wa ligi kuu
Mkwasa aliyejiuzulu uongozi Yanga mwaka jana baada ya kupata maradhi ya moyo, amesema lazima Yanga iimarishwe ili iweze kurudisha makali yake ya zamani
Mkwasa ametaka kusajiliwa kwa wachezaji ambao watarudisha utamaduni wa timu hiyo ambao ni kushambulia kupitia pembeni akimtaja Simon Msuva kuwa aliondoka na makali yake
Tangu kuondoka kwa Simon Msuva, Yanga haikuweza kuziba pengo lake na hivyo kujikuta ikikosa makali ya kushambulia kupitia pembeni
Mabao mengi ya Yanga msimu huu yamefungwa kupitia krosi au mipira iliyokufa, kiungo Ibrahim Ajib akihusika kutengeneza mabao 17 huku mwenyewe akifunga mabao sita
“Yanga inahitaji kusajili washambuliaji wa pembeni waliokuwa na uwezo kama wa Msuva au zaidi,” amesema
Mkwasa pia amependekeza maboresho kwenye safu ya ulinzi akiamini timu hiyo inahitaji angalau walinzi wawili wapya watakaoboresha eneo hilo
Eneo la mlindalango pia limempa mashaka nahodha huyo wa zamani wa Yanga ambapo amependekeza kusajiliwa kipa mwengine mwenye ubora zaidi ya waliopo
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wako katika mazungumzo na wachezaji wengi wanaotarajiwa kusajiliwa na timu hiyo
Zahera amesema kabla ya wiki ijayo kukamilika, watakamilisha usajili wa wachezaji nane