Viporo vya Simba kupangiwa ratiba maalum

Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura amesema watahakikisha ligi inamalizika mwezi ujao kama ilivyopangwa na kuhusu viporo vya Simba vitapangiwa ratiba maalum

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wambura alisema ratiba ya michezo ya Simba imekuwa na changamoto kutokana na ushiriki wa timu hiyo kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Msimu wa Ligi Kuu 2018/19 unatarajiwa kumalizika May 26 2019 huku Simba, mabingwa watetezi wakiwa bado na michezo 16 ambayo watalazimika kuicheza katika kipindi cha mwezi mmoja na siku kadhaa

“Tutafanyia kazi ratiba ya Simba ili kuhakikisha haiathiri kalenda yetu,” alisema Wambura

“Tutaandaa ratiba maalum kwa klabu ya Simba ili kuhakikisha wanamaliza michezo yao yote bila kuathiri kalenda ya TFF ambapo ligi inapaswa kumalizika mwezi Mei”

Juzi Bodi ya ligi ilisogeza mbele mchezo wa Simba dhidi ya Biashara United ili kuwapa nafasi wawakilishi hao wa nchi wafanye maandalizi ya mchezo wa pili wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe

Simba inatarajiwa kuondoka kesho Ijumaa kuelekea DR Congo tayari kwa mchezo huo utakaopigwa uwanja wa TP Mazembe keshokutwa, April 13 2019

PICHA: Man United wapoteza nyumbani dhidi ya Barcelona Champions League

Baada ya kusubiriwa kwa hamu kwa zaidi ya wiki mbili na mashabiki wa soka, hatimae usiku wa April 10 2019 katika uwanja wa Old Trafford ulichezwa mchezo wa Man United dhidi ya FC Barcelona, huo ukiwa ni mchezo wa kwanza wa robo fainali ya UEFA Champions League msimu wa 2018/2019 kwa timu hizo.

Huo ulikuwa ni mchezo wenye shauku kubwa kwa mashabiki wa Man United kwa sababu walitaka kujua na kuona timu yao ikilipa kisasi kwa FC Barcelona, baada ya kupoteza fainali mbili ya UEFA Champions League dhidi ya miamba hiyo ya Nou Camp.

Barcelona wameendeleza kuwa wababe baada ya kumfunga Man United kwa goli 1-0 lilipatikana kwa Luke Shaw kujifunga baada ya Luis Suarez kupiga kichwa alichopigiwa krosi na Lionel Messi dakika ya 12 ya mchezo, Man United kama wanataka kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo watalazimika kwenda Nou Camp wiki ijayo kupata ushindi wa kuanzia magoli 2-0, au 2-1 na kuendelea.

Mazoezi ya mwisho kabla ya kuikabili Kagera Sugar

Kikosi cha Yanga leo kimefanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa CCM Kirumba tayari kwa mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar

Mchezo huo utapigwa kesho Alhamisi katika dimba hilo

Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa kihistoria Mwinyi Zahera amesema mazoezi waliyofanya tangu jana yalikuwa ya kuondoa uchovu kwa wachezaji wake

Amesema ana matarajio kuwa vijana wake watakuwa sawa katika mchezo wa kesho baada ya kuwapa mazoezi hayo maalum

Dewji aitabiria Simba nusu fainali ligi ya mabingwa

Mfanyabiashara maarufu nchini aliyewahi kuifadhili timu ya soka ya Simba kwa mafanikio makubwa, Azim Dewji ameitabiria makubwa klabu hiyo katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwishoni mwa wiki hii huko mjini Lumbumbashi.

Dewji amesema Simba ya mwaka huu ni `moto’ na ina uwezo wa kuwang’oa Mazembe kutokana na kuundwa na wachezaji wenye vipaji na ari ya kupata matokeo chanya.

Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Dewji aliyeifikisha Simba fainali za Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 1993, alisema kitu pekee kinachopaswa kufanywa na wachezaji na viongozi wa Simba ni kuondoa mchecheto wa mchezo na badala yake kuelekeza nguvu katika mchezo wa marudiano

“Ni kweli Mazembe ni timu ngumu na kongwe. Ukiangalia ina historia kubwa Afrika na ndani ya miaka hii kumi tumeshuhudia ikitwaa ubingwa tofauti wa michuano ya CAF mara tano. Ni rekodi bora sana, lakini pamoja na ubora wao, nikiangalia ubora na uthubutu wa wachezaji wa Simba, naona vijana wetu wanaweza kufanya kweli,” Dewji amenukuliwa na Bin Zubeiry

“Wachezaji wa sasa wa Simba nawafananisha na wale wa enzi zile tunafika fainali CAF.

“Walikuwa wanajituma sana uwanjani. Na hawa ukiwaangalia wana kila kitu kinachoweza kuwaduwaza Mazembe kwao.

“Angalia walivyowakimbiza hapa Dar es Salaam, kwa kawaida Mazembe si wa kujiangusha hivyo, lakini uliona katika mchezo wa kwanza, walizidiwa sana ila bahati haikuwa kwa Simba.

“Na hata hao wanaobeza penalti ya John Bocco watambue Simba hii ni moto wa kuotea mbali na usishangae kuona mpira umetangulia Lubumbushi na wachezaji wanakwenda kumalizia kazi ya kuandika historia zaidi kwa soka ya Tanzania,” alisema

Akizungumzia tukio la klabu hiyo kupinga kubadilishiwa mwamuzi wa mchezo wa marudiano dhidi ya Mazembe, alisema jambo hilo litawarejesha mchezoni wachezaji, lakini pia kuongeza umakini wa waamuzi katika mchezo huo.

“Hata kama CAF hawatabadilisha uamuzi huo, mwamuzi aliyepangwa (Janny Sikazwe wa Zambia) atakuwa makini zaidi na kizuri ni kwamba hatataka kuharibu sifa zake zilizomwezesha kuchezesha michuano karibu yote mikubwa duniani.

“Amechezesha Kombe la Dunia mara mbili, Kombe la Mataifa ya Afrika mara mbili, pia fainali za Klabu Bingwa ya Dunia, achilia mbali hii michuano ya klabu Afrika,” alisema Dewji aliyewataka Watanzania kuendelea kuwaunga mkono wawakilishi hao wa taifa.

Katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, timu hizo hazikufungana, hivyo kuzifanya timu zote kuwa na nafasi ya kusonga mbele hatua ya nusu fainali, matokeo ya mwishoni mwa wiki yakiwa mwamuzi wa mwisho.

Simba kwenda Congo kwa Ndege ya kukodi

Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba kitaondoka Ijumaa asubuhi kuelekea Lubumbashi Congo kuifuata TP Mazembe kwenye mchezo wa marudiano robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Msafara wa Simba utajumuisha mashabiki wa timu hiyo ambao wameendelea kukamilisha taratibu za safari hiyo

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema wataondoka Ijumaa asubuhi na timu itarejea jijini Dar es salaam Jumamosi jioni baada ya mchezo

“Tutakwenda kibabe DR Congo na tutaondoka na kundi la mashabiki wetu na tutaishangaza Afrika Jumamosi ijayo, Ndege itaondoka asubuhi ya Ijumaa Aprili 12, 2019 na itarejea nchini Jumamosi jioni mara tu baada ya mchezo huo,” amesema Manara

Baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa, Simba inahitaji kushinda au hata kupata matokeo ya sare ya mabao ili iweze kusonga mbele

Mkufunzi wa Simba Patrick Aussems amesema wanayo nafasi ya kupata matokeo ugenini na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu

Hii ndio kadi rasmi ya kuichangia Yanga

Pichani juu ndio Kadi Rasmi ya Yanga na Lazima iwe na Saini kama inavyoonekana na ina namba chini kulia.

Tahadhari, asitokee mtu akakupa Kadi ili umpe fedha taslimu. Akikupa Kadi nenda kaweke Pesa Bank then mpatie Deposit Slip.

Hii ni kwa wale wanaochangia kuanzia Milioni Moja kupitia mfumo wa Kadi. Ukishadeposit tuma slip kwa namba 0716 881512