Baada ya kushushiwa lawama mashabiki kwa kikosi alichopanga kwenye mchezo wa jana, kocha Mkuu wa Taifa Stars Emmanuel Amunike amesema uamuzi wake ulitokana na mwenendo wa wachezaji mazoezini.
Jana Stars ilichapwa bao 1-0 na Lesotho katika mchezo ambao Stars ilihitaji ushindi ili iweze kufuzu kwa fainali za AFCON 2019
Amunike amesema baadhi ya wachezaji hawako katika viwango bora kama wanavyodhani mashabiki.
“Tumefanya mazoezi Afrika Kusini kwa siku 10. Nimepata muda wa kuwatathmini wachezaji wote. Lakini siwezi kutoa maelezo ya ndani zaidi kuhusu wachezaji,” amesema
“Nawapanga wale waliotayari kujitoa kwa ajili ya timu. Bahati mbaya wengine hawako katika ubora wao.
“Sina nia ya kumkosoa mchezaji yeyote. Sina tatizo na John Bocco wala Mkude, tufahamu hii ni timu ya Taifa na sio Simba”
Kocha huyo pia ameomba radhi kwa matokeo hayo ambayo hata hivyo amesema yabidi kuyakubali kwani ni sehemu ya mchezo.
Amesema Stars bado ina nafasi ya kufuzu hivyo watajipanga kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo kwenye mchezo dhidi ya Uganda utakaopigwa mwakani