Yanga 2-1 Mwadui FC

Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga leo wamedhihirisha kuwa kucheza nyumbani au ugenini hakuwezi kuwazuia kushinda baada ya kuichapa Mwadui Fc mabao 2-1 kwenye mchezo uliopigwa dimba la Kambarage mkoani Shinyanga.

Yanga iliuanza mchezo huo taratibu hata hivyo ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza mapema tu kwenye dakika ya 10 likiwekwa kambani na Mcongomani Heritier Makambo kwa shuti kali la mguu wa kushoto.

Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Mwadui Fc waliopeleka mashambulizi mengi langoni kwa Yanga. Washambuliaji wa timu hiyo walikosa ufanisi katika umaliziaji.

Kwenye dakika ya 40 mlinda lango Klaus Kindoki alifanya makosa yale yale aliyofanya kwenye mchezo dhidi ya Stand United baada ya mpira aliokuwa ameudaka kumtoka mikononi na kutua mguuni kwa Salim Aiyee aliyeifungia Mwadui Fc bao la kusawazisha.

Makosa hayo yaligharimu nafasi ya Kindoki katika mchezo huo kwani kwenye kipindi cha pili kocha Mwinyi Zahera alimtoa na nafasi yake kuchukuliwa na ‘bwa mdogo’ Ramadhani Kabwili.

Zahera pia alimtoa Gadiel Michael na nafasi yake kuingia Matheo Anthony akifanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumrudisha Jaffar Mohammed kucheza beki ya kushoto

Kwenye dakika ya 55 mpira wa adhabu uliopigwa na Feisal Salum uliwababatiza walinzi wa Mwadui Fc kabla haujatua mguuni kwa mkongwe Mrisho Ngasa aliyeutumbukiza kimiani kuihesabia Yanga bao la pili.

Hilo lilikuwa bao la tatu kwa Ngasa msimu huu.

Kwenye dakika ya 61 Zahera alifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Amisi Tambwe na kumuingiza kiungo Raphael Daudi mabadiliko ambayo yaliiongea uhai Yanga kwenye kipindi chote cha pili.

Matokeo hayo yameirudisha Yanga kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 29.