Simba 4-1 Mbabane Swallows

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba leo wametakata uwanja wa Taifa baada ya kuwafumua Mbabane Swallows mabao 4-1 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa hatua ya awali.

Ikicheza kandanda safi na la kuvutia, Simba iliwapoteza kabisa vijana hao wa Uswatini ambao huenda safari ya kuyaaga mashindano haya imewadia.

Nahodha wa Simba John Bocco ndiye aliyeanza kufungua kalamu ya mabao kwenye dakika ya 07 baada ya kufunga bao safi akiunganisha krosi ya Nicolas Gyan.

Mbabane walisawazisha bao hilo kwenye dakika ya 24 mfungaji akiwa Giovane Nzambe aliyefumua shuti kutoka nje kidogo ya 18.

Kwenye dakika ya 32 Bocco aliiongezea Simba bao la pili kupitia mkwaju wa penati baada ya Emmanuel Okwi kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na mlinda lango wa Mbabane.

Mpaka wakati wa mapumziko Simba ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1.

Kwenye kipindi cha pili Simba ilirejea na kasi iliyomaliza nayo kipindi cha kwanza.

Baada ya kosakosa nyingi, kwenye dakika ya 83 mlinda lango wa Mbabane aliirahisishia Simba kuandika bao la tatu lililowekwa kambani na Meddie Kagere baada ya kipa huyo kuteleza na kushindwa kuondosha mpira aliokuwa amerudishiwa

Hassani Dilunga aliyeingia kwenye dakika za majeruhi alimtengenezea Cletos Chama pasi mpenyezo na bila ajizi ‘CCC’ akaukwamisha mpira kimiani kuiandikia Simba bao la nne katika dakika za nyongeza

Ushindi huo unaiweka Simba katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwani inahitaji sare au isifungwe zaidi ya mabao mawili kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa huko Eswatini wiki ijayo