Simba 2-1 KMC FC :Full Time


Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba wamefanikiwa kuondoka na alama zote tatu katika mchezo wake wa kwanza wa kiporo baada ya kuilaza KMC mabao 2-1

Simba ilijipatia mabao yake yote mawili kwenye kipindi cha kwanza yakifungwa na Adam Salamba na Said Khamis Ndemla.

Salamba alitangulia kuifungia Simba bao la kuongoza kwenye dakika ya 11 akiunganisha vyema krosi ya Haruna Niyonzima aliyekuwa nahodha wa Simba kwenye mchezo huo.

Dakika tatu baadae Ndemla aliifungia Simba bao la pili akiachia shuti kali kutoka nje kidogo ya 18.

Simba iliyochezesha wachezaji wengi ambao hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza, ilicheza vizuri na kufanya mashambulizi mengi kwenye kipindi cha kwanza

Katika kipindi cha pili mabingwa hao watetezi walipunguza kasi na KMC ikatumia nafasi hiyo kurejea mchezoni na ikafanikiwa kufunga bao la kufutia machozi kwenye dakika ya 67 likifungwa na James Msuva

Kwenye mchezo huo Simba imemtumia kwa mara ya kwanza mlinzi wake mpya Zana Coulibaly aliyetua kutoka klabu ya ASEC Mimosas

Ushindi huo umeongeza hamasa kwa mashabiki wa Simba ambao Jumapili wameapa kufurika kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa kuipa sapoti timu yao itakapokuwa ikichuana na Nkana Fc katika mchezo wa ligi ya mabingwa.

Matokeo ya ushindi pia yameifanya Simba ifikishe alama 30 na imeendelea kusalia nafasi ya tatu huku bado ikiwa na michezo mitatu ya viporo