Hatuwahofii Alliance Fc, tukutane Mwanza -Dismas Ten

Misimu miwili iliyopita Yanga ilitolewa kwenye michuano ya kombe la Azam (ASFC) na Mbao Fc katika hatua ya nusu fainali ambapo mchezo ulipigwa dimba la CCM Kirumba

Yanga itarudi tena Mwanza katika uwanja huohuo kuikabili Alliance Fc lakini ikiwa ni mchezo wa hatua ya robo fainali

Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amesema hawana hofu ya kuikabili Alliance Fc kwa mara nyingine na watajiandaa kikamilifu ili waweze kushinda mchezo huo na kutinga hatua ya nusu fainali

Baada ya kukosa ushindi kwa misimu kadhaa kwenye dimba la CCM Kirumba, msimu huu Yanga imetakata katika dimba hilo kwa kufanikiwa kuzifunga Mbao Fc na Alliance

“Tunafahamu Mwanza ni pagumu, ili kupata ushindi kwenye uwanja wa CCM Kirumba unapaswa kuwa umejiandaa kwelikweli,” amesema Ten

“Msimu huu tumefanya vizuri katika michezo yote miwili tuliocheza Mwanza, naamini tunao uwezo wa kupata matokeo kwa mara nyingine”

“Tunaiheshimu Alliance, tunafahamu ni timu nzuri lakini kucheza na Yanga ni kitu tofauti”

Kama Yanga itashinda mchezo huo utakaopigwa kati ya March 25-28, kwenye hatua ya nusu fainali itachuana na mshindi kati ya Lipuli Fc dhidi ya Singida United, mchezo ambao utakuwa wa ugenini

Mchezo wa fainali utapigwa uwanja wa Ilulu mkoani Lindi mwishoni mwa msimu