ZAHERA: Michango ya Wanayanga Ipo SALAMA

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewahakikishia wapenzi, mashabiki na Wanachama wa klabu ya Yanga kuwa pesa wanazoichangia timu yao ziko salama na wapuuze taarifa zinazosambazwa zinazodai kuwa kuna fedha zimetolewa ‘kinyemela’

Akizungumza mapema leo katika mazoezi ya Yanga yanayofanyika uwanja wa chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es salaam, Zahera amesema wanaotoa taarifa hizo wana lengo la kuwavunja moyo Wana Yanga ili wasiendelee kuichangia timu yao

“Nawaambia watu wengi wanapenda timu yetu iharibike. Kuna watu wanafanya matangazo mengi ya kusema kama mchango unaofanyika viongozi wanakula pesa”

“Wanasema kuna viongozi wanakula milioni tatu, ni uongo. Hakuna hata elfu moja, senti moja ambayo inatoka katika pesa hiyo ambayo watu wanachangia.” amesema Zahera

“Hakuna hata kiongozi mmoja ambaye ana ruhusa ya kugusa iyo pesa”

Naye nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib amesema hakuna namna yoyote ambayo fedha hiyo inaweza kutolewa bila kuidhinishwa na watia saini watatu ambao ni yeye(Ajib), Kocha Mwinyi Zahera na Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh

“Kama fedha inatakiwa kutolewa ni lazima wote watatu tusaini, hivyo taarifa inayosambazwa ni uongo kwani jambo hilo haliwezekani”

Jana kupitia Redio One, mtu aliyejitambulisha kama mwanachama wa Yanga Suleiman Kato alidai kiasi cha pesa milioni tatu zilizochangwa na mashabiki wa Yanga kupitia mitandao ya simu zilitolewa kwenye mtandao husika na kuhamishiwa kwenye Bank moja iliyopo Kariakoo ambapo aliwatuhumu Kaimu katibu Omary Kaaya pamoja na Mhasibu na baadhi ya viongozi kushirikiana katika hujuma hiyo