Ajib, Tshishimbi waandaliwa mikataba mipya Yanga

Baada ya nyota wake nahodha Ibrahim Ajib na Papi Tshishimbi kuingia kwenye rada za Simba, uongozi wa Yanga umeanza mazungumzo na wachezaji hao ili kuongeza mikataba yao, imefahamika

Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya usajili ya Yanga amesema wamebaini kama watasubiri mpaka mwishoni mwa msimu ambapo mikataba yao itakuwa imemalizika kabisa, kuna uwezekano mkubwa wa kuwapoteza wachezaji hao ambao wako katika mipango ya kocha Mwinyi Zahera kwa ajili ya msimu ujao

“Ajib na Tshishimbi ni wachezaji muhimu ambao kocha anawahitaji kwa ajili ya msimu ujao. Sio hao tu, kocha ametuagiza tuhakikishe wachezaji wote anaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao hawachukuliwi na timu nyingine,” alisema Mjumbe huyo wa Kamati ya usajili ambaye hakutaka jina lake liwekwe hadharani kwa kuwa yeye sio msemaji wa Yanga

Hivi karibu imeripotiwa kuwa Simba imeanza mkakati wa kumrejesha Ajib kunako klabu hiyo aliyoikacha mwaka 2017 huku Tshishimbi akihusishwa na mabingwa hao wa ligi kuu msimu uliopita pamoja na klabu ya Azam Fc

Zahera ameuagiza uongozi wa Yanga kuhakikisha unawapa mikataba mipya wachezaji wote anaowahitaji kabla ya msimu kumalizika

Zahera amesema kusubiri mikataba ya wachezaji hao kumalizika kabisa kutaigharimu zaidi Yanga hasa kama wachezaji hao watakuwa wakiwaniwa na timu nyingine

Jana kwenye Mkutano wa viongozi wa matawi ya Yanga, Zahera alisema anakusudia kusajili wachezaji sita wa kigeni ambao mchakato wa usajili wao anakusudia kuukamilisha kabla ya msimu kumalizika

Amewataka Wana Yanga waendelee kuhamasishana katika kuichangia timu hiyo kwani fedha hizo ndizo zitakazotumika katika usajili wa wachezaji hao na wale ambao mikataba yao inaelekea ukingoni

Zahera amesema msimu ujao anataka kutengeneza kikosi imara ambacho kitaipa mafanikio Yanga kwenye ligi na michuano ya Kimataifa.

Kwa sasa Yanga inapigania kupata moja ya nafasi za kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano CAF msimu ujao

Kutimiza hilo ni lazima itwae taji la ligi kuu au kombe la FA (ASFC)