
Simba inaweza kuandika historia nyingine leo kwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu
Mashabiki wa Simba na Watanzania wote kwa ujumla wametakiwa kuiombea timu dua njema ili iweze kupeperusha vyema bendera ya nchi huko ugenini
Aidha mafanikio ya Simba kwenye michuano hii ni mafanikio ya Tanzania kwani iwapo itafanikiwa kusonga mbele, itaiongezea Tanzania alama na pengine msimu ujao nchi inaweza kuongezewa idadi ya wawakilishi kwenye michuano hiyo
Kwa sasa Tanzania ina nafasi mbili tu kwenye michuano ya CAF wakati baadhi ya nchi zina nafasi hadi nne kutokana na vilabu vyao kufanya vizuri
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema vijana wake wana ari ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo
“Hatukuja hapa kwa malengo ya kutafuta sare, tunataka kushinda mchezo huu,” amesema Aussems
Ushindi unaweza kuihakikishia Simba kutinga robo fainali kama Vital Club itashindwa kupata ushindi dhidi ya Al Ahly katika mchezo utakaopigwa mapema saa moja jioni
Lakini hata alama moja itaifaa Simba kuelekea mchezo wake wa mwisho dhidi ya Vita Club utakaopigwa uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo March 16 2019