FT : Simba 2-0 Ruvu Shooting

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wameendeleza wimbi la ushindi katika ligi baada ya leo kuibamiza Ruvu Shooting mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa

Mabao ya Simba yalipatikana kwenye kipindi cha pili yakiwekwa kambani na beki Paul Bukaba (51′) huku bao la pili likifungwa na Meddie Kagere kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 55 baada ya Adam Salamba kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake leo akiwapumzisha baadhi ya nyota waliocheza mchezo wa ligi ya mabingwa mwishoni mwa wiki

Aidha bao alilofunga Kagere leo limemfanya afikishe mabao 13 sasa akishika nafasi ya pili nyuma ya Salim Aiyee wa Mwadui Fc mwenye mabao 16

Simba inaendelea kushika nafasi ya tatu ikiwa imefikisha alama 54, alama tano nyuma ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili huku Yanga ikiongoza ikiwa na alama 67

Hata hivyo Azam Fc na Yanga zimecheza michezo saba zaidi ya Simba