NIYONZIMA: Tutacheza fainali ya ligi ya mabingwa

Kiungo Haruna Niyonzima amesema Jumamosi ya March 16 2019 ilikuwa siku ya kipekee kwake na klabu ya Simba baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Niyonzima anayetajwa kuwa nyota wa mchezo wa siku hiyo ambao Simba iliilaza AS Vita Club mabao 2-1, amefichua kuwa licha ya kupata majeraha punde tu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Emmanuel Okwi katika dakika ya 58, amesema alilazimika kuvumilia na kuhakikisha anaitumia vyema nafasi aliyopewa na kocha Patrick Aussems

“Nilijipa moyo na kusema siwezi kuruhusu majeraha haya yakanifanya nitoke nje. Nimekuwa nikijituma ili nipate nafasi kama hii,” amesema Niyonzima

“Tangu nikiwa mdogo nimekuwa na ndoto ya kucheza fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Hakuna kitakachonizuia kutimiza ndoto hiyo na pia sikuwa tayari kuwaangusha mashabiki wa Simba na Watanzania pamoja na ndugu zangu Wanyarwanda”

“Tuna nafasi ya kucheza fainali ya ligi ya mabingwa mwaka huu, bila shaka tutaweza kwani tuna kikosi cha kufanikisha hilo pamoja na mashabiki wanaotuunga mkono muda wote”