Samatta aipongeza Simba, aiombea ushindi dhidi ya TP Mazembe

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta ameipongeza klabu ya Simba kwa kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Simba imepangwa kuchuana na TP Mazembe katika mchezo wa robo fainali

Samatta ambaye kwa sasa ni kinara wa upachikaji mabao ligi kuu ya Ubelgiji akiwa na klabu ya KRC Genk, amewahi kuzitumikia Simba na TP Mazembe

Samatta aliitumikia Simba kwa muda mfupi kabla ya mabingwa hao wa Tanzania Bara kumuuza TP Mazembe ambako aliweza kupata mafanikio zaidi

Akiwa na TP Mazembe, mwaka 2015 aliweza kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la ligi ya mabingwa Afrika yeye akiibuka kuwa mfungaji bora akipachika mabao saba

Mafanikio hayo yalimpa tuzo ya Mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani

Samatta amesema kwa hatua waliyofikia Simba, wanaweza kusonga mbele zaidi kwani wanaouwezo sawa na timu nyingine wanazoshindana nazo

Licha ya kucheza TP Mazembe kwa muda mrefu, Samatta amesema angependa kuona Simba inapata ushindi katika mchezo baina ya timu hizo ili iweze kutinga nusu fainali

“Simba sio wabaya, ukiangalia wote walioingia nao katika hatua ya robo fainali, kinachowatofautisha ni uzoefu wa kucheza mashindano ya Afrika,” amesema Samatta

“Kinachotakiwa ni maandalizi mazuri na nina imani wanao uwezo wa kufika mbali kwa sababu hata hapa walipofikia ni jitihada walizofanya katika maandalizi”

“Kama Mtanzania ningependa kuona Simba inafika mbali zaidi katika michuano hii”