Aussems apewa mbinu ya kuivusha Simba dhidi ya TP Mazembe

Droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa juzi usiku, huku Simba wakirudishwa DR Congo kuvaana na TP Mazembe.

Simba wametinga hatua hiyo ya robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi D, lililoongozwa na Al Ahly, wakiifunga AS Vita ya Congo katika mchezo wa mwisho.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wataanza kibarua hicho dhidi ya wafalme hao mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe kwa kucheza mchezo wa kwanza Aprili 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

AS Vita, iliyochapwa na Wekundu hao wa Msimbazi mabao 2-1 mwishoni mwa wiki iliyopita, kama nawaona watakavyowahadithia Mazembe kilichowakuta ndani ya uwanja huo wa Taifa.

Mara ya mwisho Wekundu wa Msimbazi kukutana na Mazembe ilikuwa mwaka 2011, baada ya hapo hawajakutana tena, kutokana na timu hiyo kukosa nafasi ya kushiriki michuano hiyo kwa kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mitano.

Simba ina kila sababu ya kuutumia vyema uwanja huo wa nyumbani kama ilivyofanya kwenye hatua ya makundi ya kuhakikisha hakuna kichwa kinachotoka salama bila kunyolewa.

Basi Simba ifanye hivyo hivyo kwa Mazembe kuhakikisha haitoki na inakufa kwa kipigo cha mabao zaidi ya matatu.

Pamoja na Simba kufungwa mechi zote tatu za ugenini katika hatu ya makundi, lakini hawajafungwa nyumbani wala kutoka sare.

Walianza kuichapa JS Saoura mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kisha wakafungwa 5-0 na AS Vita nchini DR Congo na kuchapwa tena kipigo kama hicho cha 5-0 na Al Ahly ya Misri.

Katika mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly, Simba walishinda 1-0 kabla ya kupoteza 2-0 dhidi ya JS Saoura nchini Algeria na kuichapa AS Vita 2-1 Uwanja wa Taifa.

Kocha Patrick Aussems anapaswa kukumbuka kile kilichomkuta DR Congo na Misri katika mechi za makundi za ugenini.

Simba ilikwenda kucheza mechi za ugenini kama ipo nyumbani, hali iliyosababisha kuruhusu idadi kubwa ya mabao, lakini sasa Aussems anapaswa kujua hatua hii ni ngumu kidogo, maana ukifungwa mabao mengi ugenini ujue umetoka, hivyo Simba inatakiwa ishinde nyumbani kisha iende kupaki basi ugenini.

Aussems asirudie makosa ya hatua ya makundi katika kipindi hiki, bali aje na mbinu nyingine za kujilinda.

Simba haitakuwa ya kwanza kupaki basi, kwani timu kubwa hata Ulaya kama Chelsea na Manchester United ambazo zilikuwa zikinolewa na kocha Jose Mourinho zilikuwa zikifanya hivyo.

Sina wasiwasi na Simba kutumia vyema uwanja wa nyumbani, zaidi iongeze mbinu na maarifa kwa ajili ya mechi za ugenini.

Katika hatua ya makundi, Aussems alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa atashambulia mwanzo mwisho ugenini kama anavyofanya akiwa nyumbani.

Lakini lazima akumbuke kuwa nyumbani ni tofauti na ugenini na kila mtu ana mbinu za kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani.

Aussems lazima ajue, Wanasimba sasa hivi hawahitaji mbwembwe sana, wanahitaji ushindi muhimu na kutimiza ndoto zao za kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba inakutana na Mazembe ya sasa ambayo si ya kutisha sana, tofauti na ile ya zamani, ingawa bado wapo wachezaji kama Reinford Kalaba, Tresor Mputu, lakini hawana makali kama yale ya miaka ya nyuma.

Lakini ni muhimu kwa benchi hilo la ufundi kujua kwamba Mazembe haijapoteza hata mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye uwanja wao wa nyumbani kati ya michezo tisa, wakishinda saba na kutoa sare miwili.

Wakali hao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefunga mabao 24 na kufungwa matatu tu katika michezo hiyo waliyoshuka ndani ya Uwanja wa TP Mazembe.

Katika hatua ya makundi msimu huu, timu hiyo haijaruhusu kufungwa bao lolote kwenye uwanja wao wa nyumbani, walifanikiwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya CS Costantine, walishusha kipigo cha 8-0 kwa Club Africain na 2-0 dhidi ya Ismaily.

Makala hii imeandikwa na MWANI NYANGASSA kwa hisani ya Bingwa