
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uhamasishaji, amesema Waziri Mkuu amekubali kuwa mgeni rasmi wa mchezo huo na hivyo kuwataka wakazi wa jiji la Dar es salaam na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa kuungana na Waziri Mkuu katika kuipa sapoti Stars inayohitaji matokeo ya ushindi dhidi ya Uganda
Kikosi cha Stars kimeendelea kujifua katika dimba la Taifa kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa saa kumi na mbili jioni
Stars imedhamiria kuvunja rekodi ya miaka 39 ya kukosa nafasi ya kushiriki fainali za michuano ya AFCON. Inaweza kufikia malengo hayo kama itaifunga Uganda huku ikiomba Lesotho ambayo itakuwa ugenini ikichuana na Cape Verde itashindwa kupata ushindi
Uganda tayari imefuzu ikiongoza kundi L ikiwa na alama 13, Lesotho inafuatia nafasi ya pili ikiwa na alama tano sawa na Stars lakini Lesotho imeipiku Stars kutokana na faida ya kupata alama nne katika michezo miwili ambayo timu hizo zilikutana
Cape Verde inashika mkia ikiwa na alama nne lakini pia inaweza kufuzu kama Stars itashindwa kupata ushindi dhidi ya Uganda huku yenyewe ikiichapa Lesotho