Samatta aunga mkono zawadi kwa Kapombe

Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta ameungana na wadau wanaoamini beki Shomari Kapombe ambaye aliumia nchini Afrika Kusini wakati akiwa kambini na kikosi cha Stars, anastahili kupewa zawadi kama walivyopewa wachezaji wote waliyoipeleka Stars fainali za AFCON 2019

Samatta ambaye tayari amerudi Ubelgiji kuungana na KRC Genk, amesema TFF inapaswa kumjumuisha mchezaji huyo kwenye zawadi zinazotolewa kwa kuwa aliumia wakati akitimiza majukumu ya timu ya Taifa

Aidha Samatta amesema kama hilo haliwezekani basi atawashawishi wachezaji wote wagawane na Kapombe kile walichozawadiwa

Samatta amekwenda mbali zaidi kwa kusema kama hilo haliwezekani nalo basi yeye atagawana na Kapombe nusu kwa nusu zawadi alizozawadiwa kama mchezaji wa timu ya Taifa

Nae Kapombe amesema amefurahi uiona Stars inakata tiketi ya kushiriki fainali za AFCON mwaka huu

“Nimefurahi sana kama mtanzania ambaye pia nilikuwa kwenye kikosi huko nyuma licha ya kutolewa baadaye kwakuwa nisingeweza kucheza.

“Natoa pongezi kubwa kwa wachezaji wenzangu, na wale waliosaidia kufika hatua hii.

“Kwakweli ni jambo kubwa sana kutokea kwasababu ni miaka 39 nafasi hii ilikuwa haijatokea kwetu, nina furaha kubwa kwakweli”.

Kapombe amesema hali yake inaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi akitarajiwa kujiunga na kikosi cha Simba baada ya wiki tatu hadi nne