Mchezo huo utapigwa siku ya Jumapili, March 31 katika uwanja wa Jamhuri
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wamedhamiria kutetea ubingwa wao, hivyo wanahitaji kushinda mchezo huo
“Tulipoteza mechi ya kwanza na Mbao Mwanza na sasa tumejipanga kuchukua pointi hizo tatu na kuhakikisha tunaanza kuutumia vyema uwanja wetu wa Jamhuri ambao tunaanza nao katika mchezo huo,” amesema Aussems
Hata hivyo licha maboresho yaliyofanywa, uwanja wa Jamhuri bado hauko katika kiwango bora, hali itakayomfanya Aussems alazimike kubadili mbinu ili kwendana na hali ya uwanja huo
“Kutumia Uwanja wa Jamhuri kama nyumbani hatuna jinsi, kutokana na tayari uwanja wa Taifa umefungwa, lakini kuna tofauti kubwa kati ya viwanja hivi”
“Tutajiandaa kucheza kufuatana na hali ya uwanja, muhimu tunahitaji ushindi”
Aussems amesema kikosi chake kitafanya mazoezi kwenye uwanja wa Jamhuri kesho jioni na pengine Jumamosi asubuhi kabla ya kuikabili Mbao Fc Jumapili
Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 54, huku ikiwa na michezo nane kibindoni
Hesabu za kutetea ubingwa kwa kocha Aussems zinakwenda sawa mpaka sasa kwani kama Simba itashinda michezo yake yote ya viporo, itaizidi Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa alama nane