Simba kwenda Congo kwa Ndege ya kukodi

Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba kitaondoka Ijumaa asubuhi kuelekea Lubumbashi Congo kuifuata TP Mazembe kwenye mchezo wa marudiano robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Msafara wa Simba utajumuisha mashabiki wa timu hiyo ambao wameendelea kukamilisha taratibu za safari hiyo

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema wataondoka Ijumaa asubuhi na timu itarejea jijini Dar es salaam Jumamosi jioni baada ya mchezo

“Tutakwenda kibabe DR Congo na tutaondoka na kundi la mashabiki wetu na tutaishangaza Afrika Jumamosi ijayo, Ndege itaondoka asubuhi ya Ijumaa Aprili 12, 2019 na itarejea nchini Jumamosi jioni mara tu baada ya mchezo huo,” amesema Manara

Baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa, Simba inahitaji kushinda au hata kupata matokeo ya sare ya mabao ili iweze kusonga mbele

Mkufunzi wa Simba Patrick Aussems amesema wanayo nafasi ya kupata matokeo ugenini na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu