Viporo vya Simba kupangiwa ratiba maalum

Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura amesema watahakikisha ligi inamalizika mwezi ujao kama ilivyopangwa na kuhusu viporo vya Simba vitapangiwa ratiba maalum

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wambura alisema ratiba ya michezo ya Simba imekuwa na changamoto kutokana na ushiriki wa timu hiyo kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Msimu wa Ligi Kuu 2018/19 unatarajiwa kumalizika May 26 2019 huku Simba, mabingwa watetezi wakiwa bado na michezo 16 ambayo watalazimika kuicheza katika kipindi cha mwezi mmoja na siku kadhaa

“Tutafanyia kazi ratiba ya Simba ili kuhakikisha haiathiri kalenda yetu,” alisema Wambura

“Tutaandaa ratiba maalum kwa klabu ya Simba ili kuhakikisha wanamaliza michezo yao yote bila kuathiri kalenda ya TFF ambapo ligi inapaswa kumalizika mwezi Mei”

Juzi Bodi ya ligi ilisogeza mbele mchezo wa Simba dhidi ya Biashara United ili kuwapa nafasi wawakilishi hao wa nchi wafanye maandalizi ya mchezo wa pili wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe

Simba inatarajiwa kuondoka kesho Ijumaa kuelekea DR Congo tayari kwa mchezo huo utakaopigwa uwanja wa TP Mazembe keshokutwa, April 13 2019