Makambo ataja siri ya kufunga mfululizo CCM Kirumba

Kinara wa mabao wa kikosi cha Yanga Heritier Makambo amesema ubora wa uwanja wa CCM Kirumba ni moja ya sababu inayomfanya aendelee ‘kutupia mabao’ kila anashuka katika dimba hilo

Makambo amefunga mabao matano CCM Kirumba, manne akifunga kwenye michezo ya ligi na moja akifunga kwenye michuano ya kombe la FA (ASFC)

Mabao matatu ameyafunga katika michezo miwili iliyopita dhidi ya African Lyon na jana dhidi ya Kagera Sugar

“Najisikia tofauti ninapocheza kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Nadhani ubora wa uwanja unachangia mimi kufanya vizuri,” amesema

“Tumekuwa tukipata matokeo mazuri kila tunapocheza hapa, hakuna tofauti na tulivyokuwa tukicheza uwanja wa Taifa”

“Nawapongeza wachezaji wenzangu pia kwani wanachangia mimi kufanya vizuri”

Msimu huu Yanga imeshinda michezo yote ya ligi na kombe la FA iliyocheza katika uwanja wa CCM Kirumba

Aidha akizungumzia mbio za kuwania kiatu cha dhahabu, Makambo amesema ataendelea kufunga kila anapopata nafasi ili kuisaidia Yanga kupata matokeo. Ligi bado inaendelea na lengo lake ni kuendelea kufanya vizuri

Makambo amefunga mabao 15, anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora nyuma ya Salim Aiyee wa Mwadui Fc mwenye mabao 16