NIYONZIMA: Aitwa kamati ya Nidhamu SIMBA SC

Kiungo wa Simba, Mnyarwanda Haruna Niyonzima amewekwa kikaangoni baada ya kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali.

Kwa muda mrefu Niyonzima amekuwa kwenye sintofahamu na mabosi wake huku tangu alipojiunga na wenzake mazoezini hajacheza.

Niyonzima amehojiwa na Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Suleiman Kova.

Kova, ambaye amepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, aliongoza kikao hicho akiwa na wajumbe wengine wanne kwenye ukumbi wa hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Niyonzima aliitwa na kamati hiyo kwa ajili ya kuzungumza masuala ya nidhamu yake huku ikielezwa kuwa pande zote zimeshindwa kufikia mwafaka.