Mshambuliaji kinara wa mabao katika kikosi cha Simba Emmanuel Okwi, amesema moja ya sababu inayomfanya kuwa kwenye kiwango cha juu ni ushirikiano na mapenzi anayoyapata kutoka kwa wachezaji wenzake.
Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uganda amesema mbali na kufuata maelekezo ya kocha na kujituma uwanjani, lakini amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi hicho kutokana na ushirikiano uliopo kati yake na wachezaji wenzake kikosini.
Jumapili iliyopita alickeka na nyavu mara tatu kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0.
Aidha Okwi amesema mashabiki wa timu hiyo waendelee kusubiri furaha kutoka kwa wachezaji katika kila mchezo watakaocheza.
“Sehemu yoyote kukiwapo na umoja, mafanikio yanapatikana, nipo kwenye kiwango kizuri kwa sababu ya ushirikiano uliopo ndani ya Simba, lakini pia kufuata maelekezo ya kocha na kujituma uwanjani,” alisema Okwi.
Alisema ligi ni ngumu na kila timu imejipanga kufanya vizuri na wanachokifanya wao ni kujituma uwanjani na kuweka malengo ya kupata pointi tatu kwenye kila mchezo.
“Ushindi tunaoupata kwenye mechi zetu si rahisi kuupata, kila timu imejipanga na kinachotokea ni kujituma uwanjani na kufuata maelekezo ya kocha ili kupata ushindi,” alisema Okwi.
Okwi sasa amefikisha jumla ya mabao saba katika michezo 10 aliyoichezea Simba msimu huu huku akionekana kuwa na kasi kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Msimu uliopita, Okwi aliibuka mfungaji bora kufuatia kufikisha jumla ya mabao 20.
Simba, wiki hii itashuka tena uwanjani kuumana na JKT Tanzania kwenye mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga baada ya JKT kuhamishia mechi hiyo mkoani humo.