Katibu Mkuu wa zamani wa Klabu ya Simba ambaye kwa sasa amechaguliwa kuwa mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Mwina Kaduguda, amesema baada ya kupita uchaguzi sasa wana kazi ya kuitoa Simba kutoka kuwa timu kongwe na kuwa timu kubwa Afrika.
Kaduguda, ambaye ni miongoni mwa wajumbe watano waliochaguliwa kwenye uchaguzi uliofanyika Dar es Salaam Jumapili iliyopita, alisema Wanasimba wasijidanganye kuwa Simba ni timu kubwa kwa kuwa bado haijafikia kuwa timu kubwa Afrika.
“Simba ni miongoni mwa timu kongwe Afrika na si timu kubwa, haijafikia sifa za kuitwa timu kubwa, sisi viongozi tuliochaguliwa pamoja na wenzetu upande wa pili ndio tuna kazi sasa ya kuitoa Simba hapa ilipo kuelekea kuwa timu kubwa Afrika,” alisema Kaduguda.
Alisema anawashukuru Wanasimba kwa kumrejesha tena kwenye uongozi wa klabu hiyo.
“Wakati naondoka madarakani…, tuliacha Simba ikiwa na eneo la ujenzi wa uwanja Bunju, wazo la kuwa na kiwanja lilitolewa na Hassan Hasanoo kipindi cha uongozi wangu na Mwenyekiti Mzee [Hassan] Dalali, sisi tulilifanyia kazi wazo la kiwanja tukakitafuta,” alisema Kaduguda na kuongeza:
“Tuliacha la uwanja kwa uongozi uliofuata wa Aden Rage ambaye yeye sasa alianza kuulipia fedha ili sasa iwe mali ya klabu, badala yake na yeye akauachia uongozi uliofuata ambao ulikaimiwa na Salim Try Again ambaye wameanza kuujenga, uongozi ni kuachiana kijiti…, sasa tunaenda kuukamilisha na kuanza safari ya kuifanya Simba timu kubwa Afrika,” alisema Kaduguda.
Alisema atautumia uzoefu wake ndani ya Simba na kwa kushirikiana na viongozi wenzake kuipeleka Simba mbele zaidi na kuwa timu ya ushindani kwenye michuano ya Afrika.