Simba Sc: Kocha Afunguka Kuelekea Mechi Dhidi ya Big Bullet

Licha ya kuwakosa wachezaji wake 12 wa kikosi cha kwanza, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wamejiandaa kikamilifu kuikabili Nyasa Big Bullets kwenye mchezo wa kimtaifa wa kirafiki.

Kesho Ijumaa saa 12 jioni Simba itashuka kwenye uwanja wa Taifa kuchuana na mabingwa hao wa Malawi.

Aussems amesema atautumia mchezo huo kuwapa nafasi wachezaji wake ambao wamekuwa hawatumiki mara kwa mara kutokana na ushindani wa namba uliopo kwenye kikosi chake.

“Msimu huu tunakabiliwa na michuano mingi. Tunawahitaji wachezaji wetu wote wawe katika kiwango bora na tayari kuipa matokeo timu wanapohitajika,” amesema Aussems

“Mchezo wa kesho tutawakosa wachezaji wanaozitumikia timu za Taifa lakini itakuwa ni nafasi nzuri kwa wachezaji waliobaki kuonyesha uwezo wao.”

“Pia mchezo huo utawapa uzoefu wa michezo ya Kimataifa kwani tunacheza na timu ambayo ni bingwa wa nchi kama sisi”