Hatima Ya safari ya Cameroon Mikononk mwa STARS

Wakati Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Mnigeria Emmanuel Amunike, akisema haikuwa rahisi kuwafunga Cape Verde na kurejesha matumaini ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Cameroon mwakani, hesabu za Tanzania kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 ziko mikononi mwetu.

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde mwezi iliyopita, uliifanya Stars ifikishe alama tano na huenda ushindi kwenye mchezo wa keshokutwa dhidi ya Lesotho utaipeleka Stars Cameroon kutegemea na matokeo ya mchezo wa Uganda dhidi ya Cape Verde.

Kwani kama Uganda itaifunga Cape Verde itafikisha alama 13 huku Stars ikifika alama nane kama itaifunga Lesotho.

Alama hizo haziwezi kufikiwa na Cape Verde wala Lesotho hata zikishinda mchezo mmoja utakaokuwa umebaki.

Stars imeweka kambi nchini Afrika Kusini kwa takribani wiki nzima ikijiandaa na mchezo huo utakaopigwa Jumapili Novemba 18 huko Lesotho.

Kikosi cha Stars kinakwenda Lesotho bila ya nahodha wake Mbwana Samatta ambaye atakosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Amunike amesema wanakwenda Lesotho wakiwa na lengo moja tu la kuhakikisha wanaibuka na ushindi ambao utaisogeza tiketi ya kufuzu karibu zaidi.