Uganda 1-0 Cape Verde : Stars inahitaji UShindi ili kufuzu

Uganda Cranes imekuwa timu ya kwanza kundi L kufuzu kwa fainali za michuano ya AFCON 2019 baada ya kuichapa Cape Verde bao 1-0 katika mchezo wa raundi ya tano uliopigwa leo nchini Uganda.

Bao pekee la Uganda lifungwa na Patrick Henry kwenye dakika ya 78.

Uganda ilikuwa inahitaji alama moja tu kujihakikishia kufuzu.

Ushindi huo umeifanya timu hiyo ifikishe alama 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kutoka kundi L.

Matokeo hayo pia yameipa nafasi timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kuweza kufuzu kesho kama itaifunga Lesotho katika mchezo utakaopigwa Maseru.

Ushindi utaiwezesha Stars kuwa na alama nane ambazo hazitaweza kufikiwa na Cape Verde yenye alama nne wala Lesotho yenye alama mbili.