Simba sc Kuwatoa kimasomaso Watanzania Klabu Bingwa

Benchi la ufundi la Simba akili yote kwa sasa limeielekeza Mbabane Swallows kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mpango mkakati utakamilika mara baada ya wachezaji waliopo na timu zao za taifa kurejea kikosini.

Kalenda ya michuano ya Kimataifa imemalizika jana ambapo wachezaji waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kurejea kikosini kuanzia kesho.

Kocha wa Simba Patrick Aussems amesema zimebaki siku chache kabla ya mchezo huo, hivyo tayari ameanza program za kuwakabili wapinzani wao hao.

Aussems, amesema anaifuatilia Mbabane kujua uwezo na mapungufu yao.

“Kila kitu kinaenda sawa, tunaendelea na mazoezi kwa wachezaji tulionao kikosini huku tukiwasubiri waliopo kwenye timu za Taifa,” Aussems amenukuliwa na gazeti la Nipashe

Amesema mikakati yake na mbinu kamili kwa wachezaji wake zitakamilika pindi wachezaji wake waliopo timu za Taifa watakaporejea.

“Wakirejea tunaendelea na maandalizi yetu, kwa sasa naendelea na wachezaji tulionao, nashukuru kila kitu kinaenda sawa,” alisema Aussems.

Mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika umepangwa kuchezwa kati ya Novemba 27 na 28 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana Desemba 4-5, mwaka huu nchini Swaziland.

Timu itakayoibuka mshindi wa jumla itaingia kwenye hatua ya kwanza ya michuano hiyo kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu.