SIMBA : Kocha kuwaandalia Dozi Lipuli FC

Mkufunzi wa klabu ya Simba Patrick Aussems, amesema kikosi chake kimejiandaa vyema na kina matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya lipuli Fc utakaopigwa dimba la Taifa kesho Ijumaa.

Mchezo huo ni mwendelezo wa Ligi Kuu iliyokuwa imesimama kwa muda kupisha Kalenda ya Fifa ya mechi za kimataifa.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji kikosi chake kwa mara ya kwanza msimu huu kitamkosa beki mahiri Shomari kapombe aliyeumia akiwa na timu ya Taifa nchini Afrika Kusini.

“Tumejiandaa vizuri, tulikuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi kwa wachezaji ambao hawakuwapo kwenye timu za taifa, naamini bado tutaendeleza makali yetu,” amesema

Mbelgiji huyo amesema anafahamu mashabiki wa timu yake wanataka mwendelezo wa ushindi na ndicho alichokuwa akikifanyia kazi.

“Tutaingia uwanjani kwa lengo la ushindi na nafurahi kuona wachezaji wangu wanahamasa na hata wale waliokuwapo kwenye timu ya taifa nao wanauangalia mchezo huu kwa umakini,” alisema.

Mchezo huo wa kesho awali ulikuwa ufanyike juzi lakini bodi ya ligi iliusogeza mbele ili kuwapa nafasi wachezaji wa Simba waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa kuungana nao na kupata muda kidogo wa kupumzika.

Simba ilikuwa na wachezaji 10 kwenye timu za Taifa za Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi