YANGA: Kulipa kisasi Leo dhidi ya Mwadui

Baada ya kufungwa bao 1-0 msimu uliopita kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Leo Yanga inashuka tena katika uwanja huo kusaka alama tatu muhimu.
Changamoto zilizoikumba Yanga mwishoni mwa msimu uliopita zilipelekea kupoteza mchezo dhidi ya Mwadui Fc uliopigwa May 19 2018 ukiwa ni mchezo wa tatu Yanga kufungwa mfululizo baada ya pia kufungwa na Prisons na Mtibwa Sugar.
Wakati huo Yanga ilikwenda Shinyanga ikiwa na wachezaji 13 tu wa kikosi cha kwanza kilichoongozwa na aliyekuwa kocha msaidizi Shedrack Nsajigwa.
Lakini hali ni tofauti msimu huu ambapo Yanga iko mkoani humo ikiwa na kikosi chake kamili sambamba na kocha wake Mwinyi Zahera
Ni mchezo ambao Yanga inahitaji kuibuka na ushindi ili kulinda rekodi yake ya kutofungwa lakini pia kujiimarisha katika mbio za kuwania ubingwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa timu za Azam Fc na Simba
Tangu kuanza kwa msimu wa 2018/19 Yanga haijapoteza mchezo wowote katika ligi na hata michezo ya kirafiki.
Kikosi hicho cha Zahera kimeweka rekodi ya kipekee kikiwa kimecheza karibu miezi mitatu bila ya kufungwa kinyume na matarajio ya wale waliokuwa wakibeza.
Mara ya mwisho Yanga kufungwa ilikuwa August 28 kwenye mchezo wa mwisho wa kombe la shirikisho hatua ya makundi dhidi ya Rayon Sport nchini Rwanda ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0
Yanga imecheza michezo 10 kwenye ligi bila ya kupoteza ikishinda michezo nane na kutoka sare michezo miwili.
Inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 26 sawa Simba lakini Yanga ikiwa imecheza michezo pungufu