Idadi kubwa ya mashabiki wa Yanga wameungana na Watanzania wengine waliojitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam kuipa sapoti Mtibwa Sugar inayochuana na Northern Dynamo kutoka Shelisheli katika mchezo wa kombe la Shirikisho hatua ya awali.
Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0, Jaffar Kibaya akifunga mabao matatu ‘hat-trik’ huku bao la nne likifungwa na Riphat Msuya
Baadhi ya mashabiki wa Yanga wameingia uwanjani na mabango yanayobainisha kuwa uzalendo huo utaishia kwa Mtibwa Sugar leo tu lakini kwa siku ya kesho, Simba watapambana na hali yao!
Simba itashuka dimba la Taifa kesho Jumatano kuumana na Mbabane Swallows katika mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa.
Kama ilivyo kwa mashabiki wa Simba ambao hushangilia timu pinzani zinapokuja kuchuana na Yanga, kwa uzoefu uliopo, hali itakuwa hivyo hivyo kwa upande wao kesho kwa mashabiki wengi wa Yanga kuiunga mkono Mbabane Swallows.