Yanga 3-0 JKT Tanzania

Yanga imeendeleza ubabe katika ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya leo kuwafumua maafande wa JKT Tanzania kwa mabao 3-0 kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa

Vijana wa Mwinyi Zahera wamekwea kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 35 na kuipita Azam Fc yenye alama 33 huku kila timu ikiwa imeshuka dimbani mara 13.

Ushindi huo pia umeifanya Yanga izidi kuitimulia vumbi Simba iliyo katika nafasi ya tatu ikiwa na alama 27 sasa ikiwa imeachwa kwa alama nane.

Alikuwa ni Heritier Makambo aliyeanza kuifungia Yanga bao la kuongoza kwenye dakika ya 30.

Mcongomani huyo ameendeleza rekodi yake ya kupasia nyavu sasa akifunga kwenye mchezo wa tatu mfululizo leo akitumia vyema makosa ya safu ya ulinzi ya JKT Tanzania.

Hilo lilikuwa bao lake la saba msimu huu ambapo amewafikia Okwi na Kagere wote wakiwa nyuma ya Eliud Ambokile wa Mbeya City mwenye mabao nane.

Mabao mengine ya Yanga yalipatikana kwenye kipindi cha pili yakifungwa na ‘Uncle’ Ngasa (54′) na Ibrahim Ajib (79′) kupitia mkwaju wa penati baada mlinzi wa JKT Tanzania kuzuia kwa mkono shuti la Thabani Kamusoko

Ngasa na Ajib wamefikisha mabao manne kila mmoja wakizidi kupanda juu kwenye orodha ya vinara wa mabao msimu huu.

Kwa mara nyingine Yanga imedhihirisha uimara wake kwani JKT Tanzania ni moja ya timu ngumu sana kwenye ligi msimu huu