Kocha SIMBA: Ajipanga kuwaua Mbabane Kwao

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki hii kwenda Eswatini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows.

Mchezo huo utapigwa Jumatano ijayo huko Swaziland Simba ikiwa mbele kwa mabao 4-1 kufuatia ushindi iliyopata uwanja wa taifa juzi.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems ameendelea na maandalizi ya kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu.

Aussems amesema anakiandaa kikosi chake kuweza kupambana na mazingira watakayokutana nayo ugenini ili kuweza kulinda ushindi na hata kushinda ugenini.

“Ushindi tuliopata hapa nyumbani umetuweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele. Lakini bado tunapaswa kuamini kazi bado hatujaimaliza,” amesema Aussems

“Tunakwenda ugenini tukiwa na faida ya mabao matatu, tunajiandaa kikamilifu kuhakikisha tunapata matokeo ugenini yatakayo-tuhakikishia kufuzu hatua inayofuata”

Matokeo ya sare, ushindi au hata kufungwa chini ya mabao matatu yataiwezesha Simba kuitinga raundi ya kwanza ambapo itachuana na mshindi kati ya Nkana Fc dhidi ya UD Songo.