KOCHA ZAHERA ANAJUA MPIRA

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amedhihirisha yeye ni Mwalimu wa mpira baada ya kufanikisha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons leo.

Mabadiliko aliyofanya kwenye dakika ya 72 kwa kumtoa beki Juma Abdul na kumuingiza mshambuliaji Amisi Tambwe yaliwashangaza wengi tena wakati huo Yanga ikiwa nyuma kwa bao 1-0

Lakini baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika huku ubao ukisoma Prisons 1-3 Yanga, imedhihirisha Mcongomani huyo alifanya uamuzi sahihi wa kumuingiza Tambwe.

Tambwe alihusika katika mabao yote matatu, akifunga mawili huku pasi yake ikizaa mkwaju wa penati uliowekwa kambani na Ibrahim Ajib.

Zahera aliweza kusoma taswira ya mchezo huo na kubaini kuwa kumuingiza Tambwe kungeipa matokeo Yanga.

Aidha Zahera amefanikiwa kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia kiasi kwamba hawapendi kabisa kupoteza mchezo.

Upambanaji walio-onyesha kwenye kipindi cha pili unadhihirisha kuwa wachezaji wa Yanga wameiva na haitakuwa rahisi kwa timu yoyote kuifunga Yanga msimu huu.