Simba imetua salama Manzini, Eswatini na leo Jumatatu jioni inatarajia kupasha moto kwenye Uwanja wa Mavuso tayari kwa mchezo wake wa kesho Jumanne dhidi ya Mbabane Swallows, huku nyota wake wakijazwa mamilioni.
Msafara wa watu 26 wakiwamo wachezaji 20 ulipaa alfajiri ya jana Jumapili kuelekea Eswatini, lakini nyota wake wakiwamo Meddie Kagere, John Bocco na wengine wakiwekewa mezani mzigo wa maana ili kuwahamasisha waifumue tena Mbabane.
Juzi kabla ya kikosi hakijaanza safari ya kwenda Uwanja wa Ndege ili kukwea pipa kuelekea Eswatini, mabosi wa Simba wakishirikiana na bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji, waliwakalisha chini wachezaji wakiwaeleza wanataka ushindi ugenini.
Lakini ili kuhakikisha ushindi huo utakaowavusha hadi raundi ya kwanza unapatikana kirahisi, mastaa hao wakaambiwa; “Mkiachana na posho na bonasi zenu za kawaida za ushindi wa mechi za nyumbani, kuna mzigo wa maana mtaubeba kama mtashinda ugenini kama motisha kwenu.”
Kauli hiyo iliwafanya wachezaji kutabasamu na kuahidi lazima Mbabane ife, baada ya kuifumua jijini Dar es Salaam kwa mabao 4-1, kwa vile wanahitaji fedha hasa ikizingatiwa hiki ni kipindi cha kuelekea sikukuu za kuuaga mwaka 2018.
Wanene wa Msimbazi waliposikia ahadi hiyo ya ushindi kwa vijana wao wakawaambia wakipata matokeo ya kusonga mbele basi kila aliyecheza atavuna Sh 2 milioni nje ya mshahara na posho zao za kawaida.
Kama Kocha Patrick Aussems atawatumia nyota wote 20 katika mechi hiyo maana yake Simba itamwaga Sh 40 milioni kwa vijana, wale ambao hawatapata nafasi ya kucheza lakini wakavaa jezi nao watafutwa jasho.
Inaelezwa mshiko huo unajumuisha mchezo wa kwanza na huo wa kesho Manzini, hivyo kama kuna aliyecheza mechi ya Dar lakini akakosa mchezo wa Eswatini atapata nusu ya fedha watakazopewa wenzao ili iwaongeze motisha wapambane wapate nafasi ya kucheza.
Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alisema kama viongozi wamejipanga kuweka motisha kwa wachezaji wao ili wapambane na kupata matokeo mazuri ya kusonga mbele kwani timu zote dunia zinafanya vizuri kwa kuweka motisha kama hizo.
“Kama uongozi tumeanza na posho hizi ambazo nina imani katika mechi za mbele ugumu wa mashindano utaongezeka na hata posho zitakuwa kubwa zaidi ya hizi ambazo tutawapatia wakati huu,” alisema.
“Tunafanya yote haya ili kuhakikisha Simba inafanya vizuri msimu huu katika mashindano ya kimataifa ili kutimiza malengo ya kwenda kucheza hatua ya makundi,” alisema Mkwabi.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema; “Tutakuwa tunawapatia matosha wachezaji wetu tofauti na zile za kwenye ligi na tutawapatia kile ambacho tutakuwa tunawahidi kwani viongozi huo tunakutana kujadili suala hilo.”
KWASI, JUUKO WATEMWA
Katika hatua nyingine mabeki, Asante Kwasi na Juuko Murshid wameachwa kwenye safari hiyo kama ilivyokuwa kwa Haruna Niyonzima aliyekwama kwa sababu ya viza.
Kiungo Haruna Niyonzima alitakiwa kuondoka Ijumaa usiku lakini akakwama sambamba na Nicholas Gyan ambaye alfajiri ya jana alisepa na msafara huo wa Simba ukiongozwa na Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori sambamba na Mwenyekiti Mkwabi.
Kwasi na Juuko wameachwa kwa vile hawajawa fiti na Niyonzima alikiri kuachwa kwa sababu ya viza, licha alikuwa kwenye mipango ya kuwahishwa mapema na wenzake Rashid Juma na Gyan.
“Nadhani viongozi hawakufahamu kama nilitakiwa kuwa na viza ili niweze kuingia Eswatini ndio maana nimeshindwa kupata ruhusa ya kusafiri na nipo Dar naendelea na ratiba ya mazoezi,” alisema Niyonzima.
Wachezaji wengine walioachwa nchini ni Yusuf Mlipili, Marcel Kaheza, Mohammed Rashid, Ally Salim, Said Mohammed ‘Nduda’ na Abdul Selemani, huku 20 waliosafiri ni pamoja na Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, James Kotei, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga.
Wengine Deogratius ‘Dida’, Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi, Mohammed Ibrahim, Adam Salamba, Said Ndemla, Rashid Juma, Poul Bukaba, Mzamiru Yasin.