MO Akoleza Moto Ubingwa Africa

Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji ‘MO’ amewapongeza wachezaji wa timu hiyo baada ya kufanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Simba imeiondosha Mbabane Swallows katika hatua ya awali ya michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1

MO amesema ushindi wa jana ni ishara kwamba mabingwa hao wa Tanzania Bara wako tayari kupambana na vigogo wengine wa Afrika kuwania ubingwa wa bara hili

“Hongera Simba ya Africa. Sasa tuendelee na maandalizi ya mchezo unaofuatia, Mungu atutangulie. Narudia tena, lengo letu ni kuwa mabingwa wa Africa,” ameandika MO kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram

Mwanzoni mwa msimu uliopita wakati wa tamasha la SIMBA DAY, MO alitoa ahadi ya kuijenga Simba imara itakayokuwa na uwezo wa kushindana sio Tanzania pekee bali Africa nzima

Ahadi hiyo ameikamilisha kwa kiasi kikubwa kwani licha ya usajili wa wachezaji mahiri, Simba imemleta kocha Patrick Aussems ambaye ametengeneza timu imara ambayo imeonyesha kuwa tayari kuchuana na timu yoyote barani Afrika.