Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema timu yake imefuata alama tatu mkoani Shinyanga hivyo iko tayari kwa mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Stand United utakaopigwa kesho Jumapili kwenye uwanja wa CCM Kambarage
Simba iliweka kambi ya siku mbili mkoani Singida kabla ya kutua Shinyanga hapo jana
Aussems amesema anatambua mchezo huo hautakuwa mwepesi lakini kama walivyofanya katika michezo iliyopita, lengo lao ni kuondoka na alama zote tatu
Juzi kocha wa Stand United Athuman Bilali ‘Bilo’ alitamba kuwa timu yake itaibuka na ushindi katika mchezo huo ambapo alisema Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo Ndanda Fc, Mwadui Fc na timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu
“Tumewafuata Stand United, tunajua kila timu sasa inajiandaa kuonyesha ushindani itakapocheza na sisi, tunajua hilo, lakini mipango yangu ni kuhakikisha tunashinda mechi hii ya Jumapili, tuko tayari,” alisema Aussems jana baada ya kutua mkoani Shinyanga
Jana jioni kikosi cha Simba kilijifua mkoani Shinyanga kujiandaa na mchezo huo ambao ushindi utazidi kuisogeza Simba kileleni