Jumamosi ya wiki hii Simba itakuwa ugenini nchini Algeria ikichuana na JS Saoura katika mchezo ambao huenda ukaifanya Simba iandike historia nyingine barani Afrika
Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka baadae leo kuelekea Algeria ambapo Aussems amesema wanakwenda kusaka alama tatu
“Kwa nini tufikirie sare badala ya ushindi? tunaenda Algeria kupambana kupata ushindi ambao kwa kweli utakuwa umetuweka karibu kabisa na kufuzu hatua ya robo fainali ambayo ndio malengo yetu kwa sasa,” amesema Aussems.
Aussems amesema wapo tayari kwa mchezo huo kwani michezo waliyocheza karibuni katika ligi imewasaidia kujiimarisha zaidi
Baada ya mchezo dhidi ya JS Saoura ugenini, Simba itarejea nyumbani kujiandaa na mchezo wa mwisho dhidi ya AS Vita utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 19
Kama Simba itashinda mchezo huo utakaopigwa saa nne usiku halafu AS Vita Club ikashindwa kuifunga Al Ahly kwenye mchezo wa mapema utakaopigwa saa moja usiku, basi mabingwa hao wa Tanzania watajihakikishia kuwa miongoni mwa timu nane zitakazotinga robo fainali