Michango yamkatisha tamaa Zahera

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema hataendelea kubaki katika klabu hiyo kama Wana Yanga hawatajitoa kuichangia timu kwa ajili ya mipango ya msimu ujao

Akihojiwa na moja ya redio maarufu nchini, Zahera amesema amekuwa akijitoa kuisaidia Yanga na alitarajia Wana Yanga nao watafanya hivyo wakati huu ambao timu inapita katika kipindi kigumu lakini hali imekuwa tofauti

“Wanasema Yanga ni timu ya Wananchi lakini mbona wananchi hao hawaonekani kuisaidia timu?” alihoji Zahera

“Msimu huu hatukuwa na malengo ya kutwaa ubingwa, sababu iko wazi, kikosi chetu hakijakamilisha mahitaji ya kuweza kuwa mabingwa”

“Nilitegemea Wana Yanga watachangia timu kama tulivyopendekeza ili msimu ujao tuweze kuwa na kikosi imara zaidi”

“Lakini kwa hali inavyoendelea mimi sitakuwa tayari kufanya kazi kwenye timu ambayo haina malengo.”

“Sitakuwa tayari kuendelea kuwasaidia watu ambao wenyewe hawajisaidii”

Zahera amefanya kazi kubwa msimu huu ambapo licha ya mapungufu yaliyopo, ameweza kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ikipoteza michezo miwili tu

Kocha huyo Mcongomani anataka kuiona Yanga inatoka katika ‘ukata’.

Pendekezo la kuwataka Wana Yanga waichangie timu yao ni moja ya njia za muda mfupi zinazoweza kuifanya Yanga ikasimama wakati ikiendelea kuandaa mikakati ya kuweza kujitegemea kama walivyo watani zao Simba

Hata hivyo muitikio mdogo wa Wana Yanga katika kutoa michango umemfanya kocha huyo akate tamaa na pengine huenda akaondoka mwishoni mwa msimu kama mambo hayatabadilika