Aussems afunguka utayari wa kikosi cha Simba kuelekea mchezo wa kesho

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema vijana wake wako tayari kuwakabili AS Vita Club na hawana wasiwasi wowote kuelekea mchezo huo

Jana jioni Simba ilijifua katika uwanja wa Taifa yakiwa ni maandalizi yake ya mwisho katika uwanja huo kabla ya mchezo hapo kesho

Aussems amesema licha ya kuwa tayari wamefikia malengo ya msimu huu ya kutinga hatua ya makundi, lakini wana nafasi adimu ya kutinga robo fainali kama watashinda mchezo huo utakaopigwa mbele ya mashabiki wake takribani elfu 60

“Mimi nipo sawa na hata wachezaji wangu wapo vizuri, ni mechi yenye msisimko sana tunajua tukishinda tutaingia robo fainali na tumesubiri jambo hili kwa miezi 7 sasa,” amesema

“Hata kama matarajio hayakuwa makubwa sisi kufika mbali kwenye ligi ya mabingwa Afrika, lakini bado tuna nafasi kwa hiyo hatuna presha, zaidi presha ipo kwao (AS Vita) kwa sababu ni wanafainali wa kombe la shirikisho mwaka jana na kama hawatafuzu itakuwa jambo baya sana kwao.”

“Hatupo katika hali inayofanana, chochote kitakachotokea ni ziafa kwetu, tuna nafasi adimu ya kucheza mchezo huu muhimu mbele ya mashabiki 60,000 kwa hiyo itakuwa mechi nzuri na wachezaji wapo tayari.”

Mchezo huo utapigwa saa moja usiku sambamba na mchezo kati Al Ahly dhidi ya JS Saoura