Manara amtahadharisha Zahera

Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema wamebaini kocha wa Yanga Mwinyi Zahera hajasafiri na timu yake ambayo kesho inamchezo dhidi ya Lipuli Fc akibaki jijini Dar es salaam kuipokea AS Vita Club

Zahera ameonekana akiambatana na viongozi wa timu ya Vita Club itakayochuana na Simba hapo kesho

“Hii ni mechi ya kitaifa na ya kimataifa, tunaiwakilisha nchi, kuna kocha yeye kazi yake imekuwa ni kuzunguka na Vita tu na aliaga anaenda kwao Congo hata Iringa hajaenda.

“Hii ni mechi ambayo nchi inajua, Rais anajua, sasa ole wake aendelee kutuharibia mipango,” amesema Manara kwenye mahojiano yake na eFM radio

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Manara amesema kikosi kiko tayari, ari na morali ya wachezaji iko juu kuelekea mchezo huo

Amewataka mashabiki kuwahi mapema uwanja wa Taifa hapo kesho ili wawe sehemu ya historia ambayo Simba imepania kuiandika