Niyonzima ampagawisha Aussems, aapa kumbakisha Simba

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema anajivunia uwepo wa kiungo Haruna Niyonzima katika kikosi chake na amesisitiza kiungo huyo hatauzwa

Katika siku za karibuni Niyonzima ameonekana kufanya vyema hali inayoashiria amerejea katika kiwango chake cha zamani

Ukizungumzia ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Simba dhidi ya AS Vita na kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, ni lazima utaje jina la Niyonzima kwani alikuwa miongoni mwa wachezaji waliojituma zaidi katika mchezo huo

Aussems amefichua kuwa wakati alipokutana na Niyonzima kwa mara ya kwanza baada ya kuanza kuinoa Simba, alibaini kiungo huyo alikuwa amekata tamaa

Aussems amesema alifanya kazi ya ziada kumrejesha nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda katika kiwango chake baada ya kubaini ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu

Anaamini uongozi wa Simba utamuongezea mkataba kwani ni miongoni mwa wachezaji anaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao