
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mo amesema kikosi cha Simba kimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo, sehemu iliyobaki ni ya mashabiki kujitokeza kwa wingo uwanjani ili kuwaongezea wachezaji morali ya ushindi
“Tumejipanga vizuri sana, ari ya wachezaji wetu ni kubwa na Mungu akitujalia basi kesho tutafanya maajabu. Mimi kilichonileta hapa ni kuwaomba mashabiki wa Simba, Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani,” amesema Mo
“Kujitokeza kwa mashabiki kuna faida kuu mbili, moja unawaongezea nguvu wachezaji wetu na wao wanaona kuwa Watanzania wapo nyuma yao, lakini pili inawaogopesha wapinzani wetu”
Mo amesema mashabiki wa Simba wameifanya timu hiyo iandike rekodi ya kuwa timu namba moja kwa kujaza uwanja katika michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu
“Niwashukuru mashabiki wa Simba, niwapongeze ukiangalia takwimu za mechi za Ligi ya Mabingwa hakuna timu ambayo imejaza uwanja wake kama Simba Sports Club, Simba inaongoza kwa kujaza uwanja kwenye mechi zake”
“Nawaomba sana mashabiki ikitokea bahati mbaya ya hapa na pale, tuendelee kushabikia sio tu mpaka tukipata goli, naomba sana tubadilike kwenye hilo, tushangilie Simba tangu mwanzo hadi mwisho”
“Hapa hatushiriki tu, tunajiamini kwamba tunaweza na tunataka kwenda mbali zaidi ya hapa”
“Shabaha yetu sio tu kufanikiwa mwaka mmoja, tunataka kushinda kombe kila mwaka ili tushiriki Ligi ya Mabingwa kila mwaka, tunataka kushinda kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika, mimi naamini uwezo tunao, tumtangulize Mungu”