Bocco asilaumiwe kwa kukosa penati – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema matokeo ya suluhu waliyopata dhidi ya TP Mazembe jana yalitokana na timu hiyo kukosa bahati na hakuna jambo jengine

Aussems amesema wachezaji wake jana walicheza kama alivyowaelekeza walitengeneza nafasi nyingi, lakini walikosa bahati

Akizungumzia tukio la nahodha John Bocco kukosa mkwaju muhimu wa penati ambayo huenda ingeiweka Simba katika mazingira mazuri ya kuibuka na ushindi, Aussems amesema Bocco hawezi kulaumiwa kwa kukosa penati kwa kuwa hiyo ni sehemu ya mchezo

“Huwezi kumlaumu mchezaji kwa kukosa penati kwani, hilo ni pigo la bahati pia,” alisema

“Wachezaji wote duniani huwa wanakosa penati hivyo hapaswi kulaumiwa”

Nae msemaji wa Simba Haji Manara amewashukia baadhi ya mashabiki wa timu hiyo ambao wamemshambulia Bocco baada ya mchezo wa jana

Manara amesema Bocco ndiye mchezaji ambaye yuko katika kiwango bora zaidi katika kikosi cha Simba kwa sasa

Kwa siku za karibuni Bocco ameifungia Simba mabao mengi kwenye ligi pamoja na kutoa pasi muhimu bila kusahau amekuwa na rekodi nzuri ya kufunga mikwaju ya penati

“Kumlaumu Bocco kwa kukosa mkwaju wa penati kunasababisha na ugeni wa baadhi ya mashabiki kwenye soka,” amesema Manara

“Bocco huyu ndiye anayefunga penati nyingi za Simba. Hata tulipocheza na Nkana kule Kitwe Zambia, ni Bocco aliyefunga penati muhimu ambayo baadae ilitusaidia kupata matokeo ya kuingia hatua ya makundi”

“penati ni pigo la bahati na halina mwenyewe”