Aussems atamba, hajawahi kupoteza robo fainali, aahidi ushindi Congo

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema kuwa katika historia yake ya kufundisha soka, hajawahi kushindwa baada ya kutinga robo fainali.

Aussems ambaye msimu huu amevuka malengo kwa kuipeleka Simba robo fainali, amesema baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya TP Mazmebe kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana, anaamini mchezo wa marudiano utakaopigwa April 13 Simba ina nafasi ya kushinda kama ilivyo kwa wapinzani wao TP Mazembe

“Katika historia yangu ya soka na timu ambazo nimewahi kufundisha, nilizivusha hatua ya robo fainali, ndio maana sina hofu na hili kwa uwezo wa Mungu tutafanikiwa,” amesema.

Aussems amesema anatambua ni makosa madogo waliyoyafanya katika mchezo wa kwanza na kwamba amejipanga kikamilifu kukabiliana na mchezo huo.

“Natambua kuwa Watanzania na mashabiki wa Simba walikuwa na hofu pengine tungefungwa mabao mengi na TP Mazembe katika mchezo uliopita, lakini wameshuhudia namna tulivyopambana, sidhani kama tunaweza kushindwa mchezo wa marudiano.

“Pengine hofu kubwa ni kwa sababu tutakuwa ugenini, mimi naamini kuwa mpira ni dakika 90, hata tuwe wapi ni plani yangu na juhudi za wachezaji ndizo zitakazoleta matokeo mazuri,” alisema Aussems.