Ni mchezo wa jasho na damu – Manara

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka mapema kesho Ijumaa kuelekea DR Congo tayari kwa mchezo wa pili wa robo fainali ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya TP Mazembe

Manara amesema Simba inakwenda Congo kupambana na watahakikisha wanaiwakilisha vyema nchi kwa kupata matokeo mazuri katika mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye uwanja wa TP Mazembe

Amesema wachezaji wa Simba wako tayari kuandika historia nje ya nchi

“Tunakwenda kesho kibingwa tukiwa hatuna cha kupoteza ila tunawaahidi jasho jingi litamwagika kuipigania Simba na nchi Jumamosi,” amesema Manara

“Hatuogopi lolote toka Mazembe pamoja na kuwapa heshima yao kama klabu kubwa”

“Wachezaji wetu wapo tayari kuionyesha Afrika ubora wao na ukubwa wa Simba. Tuombeeni tufike salama na turejee salama kifua mbele”

Simba inakwenda Congo kwa usafiri wa ndege maalum ya kukodi na itarejea nchini Jumamosi jioni baada ya mchezo